Wakenya wanakabiliwa na mzigo mkubwa zaidi wa kiuchumi iwapo mapendekezo ya bajeti ya mwaka wa kifedha 2026/27 yatapitishwa, kwa mujibu wa kiongozi wa Chama cha Democracy for the Citizens (DCP), Rigathi Gachagua.
Akizungumza kuhusu bajeti ya shilingi trilioni 4.82 na Mswada wa Fedha 2026, Gachagua amesema hatua za kuongeza ushuru na kuendelea kukopa zitawaathiri zaidi wananchi wa kawaida, wafanyabiashara wadogo, wakulima na vijana wanaotafuta ajira.
Amedai kuwa sekta muhimu kama afya, elimu na kilimo zimepewa fedha zisizotosheleza mahitaji ya wananchi huku serikali ikiendelea kuongeza deni la taifa.
Aidha, amepinga mapendekezo ya ushuru mpya ikiwemo VAT ya asilimia 16 kwa huduma za kidijitali na ongezeko la ushuru wa bidhaa za simu, akisema hatua hizo zitaongeza gharama za maisha na kuathiri biashara pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu.
Gachagua ameishauri serikali kuelekeza rasilimali zaidi katika uzalishaji wa chakula, afya, elimu na ajira kwa vijana badala ya kuongeza ukopaji na matumizi ya utawala.
