Serikali ya Kaunti ya Turkana kwa ushirikiano na shirika la Catholic Relief Services imezindua awamu ya pili ya kampeni ya kuzuia malaria kwa watoto.
Kampeni hiyo itatekelezwa katika maeneo ya Kakuma na Kalobeyei kabla ya msimu wa maambukizi ya malaria kati ya mwezi Juni na Oktoba.
Meneja wa Shirika la CRS nchini, Margaret Kahiga, amesema mpango huo unatumia mbinu inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani ili kulinda watoto dhidi ya malaria wakati wa msimu hatari.
Kwa mujibu wa maafisa wa afya, zaidi ya watoto elfu 132 wanatarajiwa kufaidika na kampeni hiyo huku dawa za kuzuia malaria zikipatikana kupitia msaada wa Marekani.
Naibu Gavana wa Turkana, Daktari John Erus, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na matumizi ya takwimu sahihi katika kuboresha afya ya umma.
