Wakazi wa Garissa wameeleza wasiwasi wao kufuatia kuongezeka kwa visa vya uhalifu vinavyotekelezwa na makundi ya vijana wenye silaha za jadi pamoja na baadhi ya waendesha bodaboda.
Makundi hayo yanadaiwa kuendesha wizi wa kutumia nguvu, mashambulizi na hata kuweka vizuizi haramu usiku ili kuwatoza wakazi fedha.
Matukio ya hivi karibuni yamewalazimu wafanyabiashara wengi kufunga biashara zao mapema kwa hofu ya usalama.
Kisa kilichozua hasira zaidi ni mauaji ya mtalii mmoja raia wa Marekani aliyedungwa kisu baada ya kukataa kuibiwa simu yake katika eneo la Bula Mzuri.
Baada ya mkutano wa viongozi wa kaunti na maafisa wa usalama, Gavana Nathif Jama alikosoa vyombo vya usalama kwa kuchelewa kuwakamata wahalifu wanaojulikana.
Naye Naibu Kamishna wa Kaunti, Sebastian Okiring, ameahidi operesheni maalum ya kuwaondoa wahalifu wanaojificha katika sekta za bodaboda, tuk-tuk na teksi.
