Kuongezeka kwa visa vya mauaji, wizi na mashambulizi katika Mji wa Garissa kumezua hofu miongoni mwa wakazi na viongozi. Gavana Nathif Jama ameonya kuwa hali hiyo inatishia sifa ya Garissa kama mojawapo ya miji salama nchini.
Kutokana na ongezeko la uhalifu katika miezi ya hivi karibuni, viongozi wa serikali, maafisa wa usalama, viongozi wa kidini na wawakilishi wa jamii walikutana kujadili hatua za kurejesha usalama.
Mkutano huo ulifanyika baada ya matukio kadhaa ya uhalifu kuripotiwa, likiwemo tukio la kuuawa kwa Osman Aweis, raia wa Marekani mwenye asili ya Kisomali, aliyedaiwa kushambuliwa na wahalifu waliomtaka simu yake kabla ya kumchoma kisu.
Gavana Jama ameitaka serikali ya kitaifa kuongeza maafisa wa usalama katika mji huo na kuharakisha kufunguliwa kwa vituo vya polisi vya Kunaso na Burburis ili kusaidia kukabiliana na ongezeko la uhalifu.
