Ruto: Aeleza Sababu ya Kituo cha Ebola

Kiongozi wa taifa ametetea mpango wa serikali wa kujenga kituo cha kuwatenga watu walioathiriwa na virusi vya Ebola katika Kaunti ya Laikipia, akisema hatua hiyo inalenga kuimarisha afya ya umma na uwezo wa Kenya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Akizungumza na wanahabari katika Ikulu Ndogo ya Wajir, Rais Ruto alisema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya mikakati ya kujiandaa na changamoto za kiafya zinazoweza kujitokeza siku zijazo.

Rais huyo alifananisha mpango huo na hatua zilizochukuliwa wakati wa janga la Covid-19, ambapo vituo maalum vya kuwatenga wagonjwa vilianzishwa ili kusaidia kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Kauli yake inajiri siku chache baada ya Mahakama Kuu kusitisha kwa muda ujenzi wa kituo hicho pamoja na kuwasili kwa watu walioambukizwa Ebola nchini, hadi kesi iliyowasilishwa na Katiba Institute itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Ruto aliwataka viongozi na wadau mbalimbali kuepuka kuingiza siasa katika masuala ya afya ya umma, akisisitiza kuwa serikali imejizatiti kulinda maisha ya Wakenya.

Aidha, alisema serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuzuia, kugundua na kudhibiti visa vya magonjwa hatari, huku ikiendelea kuimarisha uwezo wa taifa wa kukabiliana na dharura za kiafya kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *