Wakazi wa kijiji cha Hidabo kisiwani Lamu wameeleza hofu yao kuhusu athari za kiafya zinazodaiwa kusababishwa na moshi na harufu kali kutoka kwa tanuri ya kuchomea taka za hospitali kuu ya rufaa ya King Fahd.
Kijiji hicho chenye zaidi ya wakazi 500 kinapakana na hospitali hiyo, huku wakazi wakisema moshi unaotoka kwenye mtambo huo umeanza kuwaathiri kiafya.
Mkazi mmoja, Bi Fatma Alwy, alisema wengi wao wamekuwa wakikumbwa na matatizo ya kupumua kutokana na hewa yenye harufu kali na kemikali inayotoka kwenye tanuri hilo.
Mzee wa kijiji hicho, Bw Swaleh Babu, alisema wakazi wengi wamejitokeza kulalamikia hali hiyo na kuhoji iwapo tathmini ya athari za mazingira ilifanywa kabla ya mtambo huo kujengwa.
Wakazi pia wamedai kuwa wanawake wajawazito ni miongoni mwa walioathirika zaidi na moshi huo.
Mtetezi wa haki za binadamu Ahmed Famau alitoa wito kwa serikali kuwapatia matibabu ya bure wakazi walioathirika pamoja na kuwafidia kwa madhara yaliyosababishwa.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Lamu ambaye pia ni Waziri wa Afya wa kaunti hiyo, Dkt Mbarak Salim, alikiri kuwepo kwa matatizo ya moshi kutoka kwa tanuri hilo lakini akasema tayari limefanyiwa marekebisho.
Aidha, afisa wa mazingira Dickson Mbuthia aliwataka wasimamizi wa hospitali kote nchini kuhakikisha wanatumia mbinu salama za uchomaji taka za kimatibabu ili kulinda afya ya wananchi na mazingira.
