Mahindi ya Nchi Jirani Yawaumiza Wakulima

Wakulima wa mahindi nchini Kenya wanakabiliwa na changamoto ya wafanyabiashara wengi, kuagiza mahindi kutoka nje ya nchi kufuatia kuongezeka kwa uagizaji wa mahindi ya bei nafuu kutoka mataifa ya COMESA, hali inayozua mjadala kuhusu mustakabali wa uzalishaji wa chakula nchini.

Bei ya gunia la mahindi imeshuka kutoka takriban Shilingi 4,600 hadi karibu Shilingi 4,000 ndani ya kipindi cha miezi miwili iliyopita, jambo ambalo limeathiri wakulima waliokuwa wamehifadhi mazao yao wakisubiri bei kupanda zaidi.

Wataalamu wa sekta ya kilimo wanasema ongezeko la uzalishaji katika nchi jirani kama Tanzania, Uganda, Zambia, Malawi, Angola na Mozambique kumeongeza usambazaji wa mahindi katika ukanda huo, huku Kenya ikiendelea kuwa soko kubwa kutokana na matumizi makubwa ya unga wa mahindi.

Hali hiyo imeleta nafuu kwa baadhi ya watumiaji baada ya bei ya unga kutulia katika maeneo mbalimbali, lakini wadau wa sekta ya nafaka wanaonya kuwa kushuka kwa bei kunaweza kuwakatisha tamaa wakulima wa ndani na kuathiri uzalishaji wa baadaye.

Wachambuzi wa uchumi wa kilimo wanasema changamoto hiyo imeibua mjadala kuhusu namna ya kusawazisha biashara huria ya kikanda na ulinzi wa wakulima wa ndani dhidi ya ushindani wa bidhaa za bei ya chini kutoka nje.

Katika maeneo ya uzalishaji mkubwa kama Uasin Gishu, Trans Nzoia, Nandi, Bungoma na Nakuru, baadhi ya wakulima wanasema wamelazimika kuuza mahindi yao kwa bei ya chini kutokana na hofu ya kuendelea kwa kushuka kwa soko.

Serikali kwa upande wake imesema inaendelea kununua mahindi kwa ajili ya kuongeza akiba ya taifa, huku ikisisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *