Trump ataka mataifa zaidi kujiunga kwenye Mkataba wa Abraham

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema makubaliano yoyote ya kumaliza mzozo na Iran yanapaswa kujumuisha nchi zaidi kwenye Makubaliano ya Abraham, yaliyosimamiwa na Marekani.

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema makubaliano yoyote ya kumaliza mzozo na Iran yanapaswa kujumuisha nchi zaidi kwenye Makubaliano ya Abraham, yaliyosimamiwa na Marekani kwa ajili ya kuimarisha uhusiano kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu.

Trump amesema mazungumzo yanaendelea vizuri na amezitaja Saudi Arabia, Qatar, Pakistan, Uturuki, Misri na Jordan kama nchi zinazopaswa kujiunga haraka na makubaliano hayo.

Hata hivyo, Saudi Arabia imesisitiza kuwa itahitaji kwanza kuona njia wazi ya kuanzishwa kwa taifa la Palestina kabla ya kuhalalisha uhusiano na Israel. Pakistan nayo imesema msimamo wake haujabadilika na bado haina mahusiano ya kidiplomasia na Israel

Pendekezo la Trump limeibua pia mjadala ndani ya chama chake cha Republican, na linaweza kuongeza ugumu katika mazungumzo yanayoendelea kuhusu Iran na usalama wa Mashariki ya Kati.