Serikali ya Sudan Kusini imebadili msimamo wake na kuachana na mpango wa kuondoa vifungu muhimu kutoka kwa Makubaliano ya Amani ya mwaka 2018.
Hatua hiyo imekuja baada ya shinikizo kutoka kwa mashirika ya kiraia na mabalozi mbalimbali wa kigeni, ambao walieleza wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa kuyumba kwa mchakato wa amani na taasisi za mpito nchini humo.
Kufuatia hali hiyo, marekebisho yenye utata zaidi yameondolewa kwenye rasimu ya sheria inayojadiliwa bungeni.
Mabadiliko hayo yalitangazwa baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri uliofanyika Mei 22. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, rasimu ya sheria ya kurekebisha makubaliano hayo haitapendekeza tena kuondolewa kwa vifungu viwili vinavyotambua ukuu wa makubaliano ya amani dhidi ya sheria nyingine zote.
Mkurugenzi wa shirika la kiraia la CEPO, Edmund Yakani, amekaribisha kile alichokiita “mwitikio chanya” wa serikali, lakini amesisitiza haja ya kujitolea kikamilifu katika kutekeleza mabaki ya makubaliano ya amani.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa mwaka 2018 yanaweka bayana mchakato wa kuelekea uchaguzi na kukamilisha kipindi cha mpito.
Hata hivyo, ucheleweshaji mkubwa umesababisha serikali kuangalia njia mbadala za kuharakisha mchakato huo.
Muswada unaojadiliwa bungeni unapendekeza kuahirishwa kwa uandishi wa katiba ya kudumu pamoja na sensa ya wananchi hadi baada ya uchaguzi.
Kwa upande wake, chama cha Makamu wa Rais Riek Machar kimeendelea kupinga muswada huo, kikisisitiza kuwa vifungu vinavyotambua ukuu wa makubaliano ya amani lazima vibaki kama vilivyo.
Chama hicho pia kimeitaka serikali kuondoa muswada huo na kuanza tena mazungumzo jumuishi kabla ya kuwasilishwa bungeni.
