Martha Koome amewataka mawakili wapya walioapishwa kutumia taaluma yao kama chombo cha kuimarisha haki, kulinda Katiba na kuwahudumia Wakenya wote bila ubaguzi, hususan watu wasiokuwa na uwezo wa kifedha na wanaoishi katika maeneo yaliyotengwa.
Akizungumza Jumatatu wakati wa hafla ya kuwaapisha mawakili hao wapya, Koome alisema kuwa jukumu la wakili halipaswi kuishia tu mahakamani bali linapaswa kuwa sehemu ya kuleta matumaini, usawa na haki kwa jamii. Alisisitiza kuwa taaluma ya sheria ni wito wa kuhudumia wananchi kwa uadilifu na uwajibikaji mkubwa.
Jaji Mkuu huyo aliwakumbusha kuwa nyuma ya kila faili la kesi kuna maisha ya watu wenye changamoto halisi, wakiwemo wajane wanaopigania haki ya kumiliki mali, watoto wanaohitaji ulinzi wa kisheria pamoja na wananchi wanaojitetea dhidi ya dhuluma na unyanyasaji. Kutokana na hilo, aliwahimiza kutoa uwakilishi wa kisheria wenye huruma, heshima na maadili ya juu ili kudumisha imani ya wananchi kwa mfumo wa sheria.
Koome pia aliwahimiza mawakili hao kukumbatia mifumo ya upatanishi na njia mbadala za kutatua migogoro ili kusaidia kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa haraka zaidi. Aliongeza kuwa matumizi ya njia hizo yanaweza kusaidia kujenga maridhiano na kuimarisha mshikamano katika jamii.
