Naibu Waziri Mkuu wa Kwanza, Musalia Mudavadi, amewataka Wakenya kufuata kikamilifu maelekezo ya Wizara ya Afya kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Amesema ingawa Kenya bado haijathibitisha kesi yoyote ya Ebola, wananchi wanapaswa kuwa makini na kuchukua tahadhari kama ilivyokuwa wakati wa COVID-19 ili kulinda taifa lisikumbwe na maambukizi.
Shirika la afya la Umoja wa Afrika limeonya kuwa nchi 10 barani Afrika ziko katika hatari ya kuathirika zaidi ya Uganda na DRC.
DRC ilitangaza mlipuko wa Ebola Mei 15, unaosababishwa na aina ya Bundibugyo ambayo bado haina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa. Takwimu zinaonyesha vifo 204 kati ya visa 900 vinavyoshukiwa katika majimbo matatu.
Nchini Uganda, visa vipya vitatu vimethibitishwa, na kufanya jumla kufikia maambukizi matano, hali inayoibua wasiwasi wa kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo.
Wizara ya Afya inasisitiza uangalifu, usafi, na kufuata maelekezo ya kinga ili kuzuia mlipuko kuingia Kenya.
Serikali inawahimiza wananchi kuepuka taarifa za uvumi, kuripoti dalili zinazoshukiwa mapema katika vituo vya afya, na kusaidiana kulinda jamii hasa mipakani na maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu.
