Mahakama yasitisha amri ya kutotoka nje Lamu

Makundi ya kutetea haki za binadamu mjini Mombasa pamoja na viongozi wa kaunti ya Lamu, wameitaka serikali kuondoa mara moja amri ya kutotoka nje usiku iliyowekwa tangu mwaka 2017 kufuatia uamuzi wa mahakama uliositisha utekelezaji wake.

Uamuzi huo ulitolewa Mei 21, 2026 na mahakama kuu ya Garsen, iliyosimamisha utekelezaji wa amri hiyo katika kaunti za Lamu, Garissa na Tana River hadi kesi inayopinga uhalali wake itakaposikizwa.

Wito huo umejiri huku kukiwa na malalamishi kutoka kwa wakazi, wasafiri na wafanyabiashara kuhusu vizuizi vya barabarani na ukaguzi wa magari unaoendelea licha ya amri ya mahakama. Wamelalamikia kucheleweshwa kwa safari, kuathirika kwa biashara na kuongezeka kwa hofu ya usalama katika eneo hilo.

Hata hivyo, idara ya usalama ilisema hatua hiyo bado ni muhimu kwa ajili ya kuwalinda wananchi dhidi ya mashambulizi ya majambazi ambao wakati mwingi hushukiwa kujificha katika msitu wa Boni.

Wanaharakati wa haki za binadamu wameikosoa serikali kwa kuendelea kutekeleza amri hiyo wakisema ni ukiukaji wa haki za kikatiba na kuitaka serikali kuheshimu uamuzi wa mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *