Viongozi wakuu wa chama cha ODM Jumapili wanatarajiwa kukutana Kisumu katika mkutano mkubwa wa kisiasa unaolenga kutoa mwelekeo wa kisiasa wa jamii ya Waluo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Mkutano huo, uliopewa jina la ‘Azimio la Waluo’, unatazamwa kama moja ya mikutano muhimu zaidi katika historia ya siasa za Nyanza tangu kifo cha aliyekuwa kinara wa ODM Raila Odinga mnamo Oktoba mwaka 2025.
Kifo cha Bw Odinga kilisababisha pengo kubwa kisiasa na kuzua mvutano wa uongozi ndani ya chama hicho, huku makundi mawili ya Linda Ground na Linda Mwananchi yakijitokeza kupigania ushawishi wa kisiasa ndani ya ODM.
Kundi la Linda Ground linaongozwa na Oburu Oginga huku lile la Linda Mwananchi likiongozwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.
Sasa viongozi wa chama pamoja na maafisa wa serikali wanatarajiwa kutumia mkutano huo kujaribu kuunganisha jamii ya Waluo na kuhimiza ushirikiano wa kisiasa kati ya ODM na serikali ya Kenya Kwanza chini ya Rais William Ruto.
Dalili zinaonyesha kuwa mkutano huo unaweza kutumika kuhamasisha jamii ya Waluo kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Miongoni mwa viongozi wanaotarajiwa kuhudhuria ni Oburu Oginga, Simba Arati, Abdulswamad Nassir, Gladys Wanga, John Mbadi, Opiyo Wandayi na Hassan Joho.
Hata hivyo, mkutano huo tayari umeanza kuzua mvutano miongoni mwa baadhi ya viongozi wa Nyanza wanaopinga ushirikiano kati ya ODM na serikali ya Rais Ruto.
Gavana wa Siaya James Orengo ni miongoni mwa viongozi wanaoegemea upande wa Linda Mwananchi unaopinga mpango wa kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi ujao.
Viongozi wengine wa ODM wameeleza kuwa mkutano huo utasaidia kutoa mwelekeo rasmi wa kisiasa kwa jamii ya Waluo huku ukilenga kuimarisha umoja ndani ya chama hicho.
