Mahakama Kuu imeizuia kwa muda serikali kuanzisha au kuendesha vituo vya karantini, kutenga au kutibu wagonjwa wa Ebola nchini chini ya makubaliano yoyote na Marekani au taifa lingine la kigeni.
Mahakama pia imepiga marufuku kuingizwa nchini, kuhamishwa au kupokelewa kwa watu walioathiriwa au kuambukizwa Ebola hadi kesi hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya mahakama kuthibitisha kuwa kesi iliyowasilishwa ni ya dharura. Mlalamishi anapinga madai ya kuwepo kwa makubaliano kati ya Kenya na baadhi ya serikali za kigeni kuhusu usimamizi wa wagonjwa wa Ebola.
Mahakama imeagiza mlalamishi kuwahudumia wadaiwa nyaraka za kesi ndani ya saa 24, huku wadaiwa wakitakiwa kuwasilisha majibu yao ndani ya saa 48 baada ya kupokea nyaraka hizo.
Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani kwa maelekezo zaidi baada ya pande zote kutimiza masharti yaliyowekwa. Kwa sasa, mipango yote ya serikali kuhusu vituo vya Ebola au kuwapokea watu walioathiriwa na virusi hivyo imesimamishwa hadi mahakama itakapotoa uamuzi baada ya kusikiliza pande zote.
