Wanahabari katika Kaunti ya Wajir wamehimizwa kutumia majukwaa yao kupambana na ukeketaji, ndoa za mapema na mila nyingine zinazokiuka haki za watoto wa kike.
Wito huo ulitolewa wakati wa kongamano la wanahabari lililoandaliwa na Kenya Alliance for Advancement of Children kupitia mpango wa Future4Binti, unaotekelezwa katika kaunti za Wajir na Mandera kati ya mwaka 2026 na 2030.
Akizungumza katika mkutano huo, Timothy Ikesa alisema vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kuelimisha jamii na kubadili mitazamo kuhusu masuala yanayowahusu watoto.
Kwa upande wake, Afisa wa Uratibu wa Serikali za Kaunti Bash Mohamed aliwataka wanahabari kuripoti kwa uwajibikaji na kuzingatia maslahi ya watoto.
Washiriki waliahidi kuendeleza kampeni za uhamasishaji kwa lengo la kulinda na kuwawezesha watoto pamoja na wasichana katika eneo la Kaskazini mwa Kenya.
