Maelfu ya wafanyakazi nchini wanatarajiwa kunufaika baada ya serikali kuanza kutekeleza rasmi nyongeza ya mshahara wa chini iliyotangazwa wakati wa sherehe za Leba Dei mwaka huu.
Chama cha Wafanyakazi nchini COTU kimekaribisha hatua hiyo baada ya Wizara ya Leba kuchapisha kwenye Gazeti Rasmi la Serikali nyongeza ya mshahara wa asilimia 12 kwa wafanyakazi wa kawaida na asilimia 15 kwa wafanyakazi wa sekta ya kilimo.
Katibu Mkuu wa COTU, Francis Atwoli, amesema utekelezaji wa nyongeza hiyo ni hatua muhimu katika kuboresha maisha ya wafanyakazi wenye kipato cha chini ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto za gharama ya juu ya maisha.
Hata hivyo, Atwoli ameisisitiza Wizara ya Leba kuimarisha ukaguzi ili kuhakikisha waajiri wote wanatekeleza agizo hilo na wafanyakazi wanapata stahiki zao kikamilifu.
