Kesi Ya Gachagua Yasubiri Uamuzi Wa Mahakama Leo

Macho ya Wakenya leo yanaelekezwa katika Mahakama Kuu ya Nairobi, ambapo uamuzi wa kesi inayopinga kuondolewa afisini kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua unatarajiwa kutolewa.

Jopo la majaji watatu; Erick Ogola, Antony Mrima na Freda Mugambi, linatarajiwa kutoa uamuzi huo siku chache baada ya pande zote zinazohusika kukamilisha mawasilisho yao tarehe 22 mwezi uliopita.

Uamuzi huo unasubiriwa kwa hamu na wengi kutokana na athari zake katika siasa za taifa, hasa wakati ambapo shughuli za kisiasa zimeanza kushika kasi kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Hata hivyo, Gachagua amesema ataheshimu uamuzi wa mahakama bila kujali matokeo yatakayotolewa. Aidha, amedokeza kuwa yuko tayari kukata rufaa iwapo hataridhishwa na uamuzi huo.

Akizungumza Jumapili katika Kanisa la PCEA Muteero, Karen, kiongozi huyo wa chama cha DCP aliwataka wafuasi wake kudumisha amani na utulivu bila kujali uamuzi utakaotolewa.

Gachagua aliondolewa afisini Oktoba 17 mwaka 2024 baada ya Seneti kuthibitisha mashtaka yaliyowasilishwa dhidi yake na Bunge la Taifa.

Kupitia kesi yake mahakamani, anadai kuwa mchakato wa kumng’oa madarakani ulikiuka Katiba na kwamba hakupatiwa haki ya kusikilizwa ipasavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *