Wazazi na jamaa za wasichana 16 waliofariki katika mkasa wa moto katika Shule ya Wasichana ya Utumishi bado wanasubiri kukabidhiwa miili ya wapendwa wao.
Familia hizo zimeelezwa kuwa zitasubiri hadi Juni 17 mwaka huu kabla ya miili hiyo kukabidhiwa kufuatia mipango ya ibada ya pamoja.
Huzuni ilitanda katika makafani ya Naivasha baada ya matokeo ya uchunguzi wa DNA kuthibitisha utambulisho wa miili ya wanafunzi hao.
Baadhi ya wazazi wameeleza kutoridhishwa kwao na hatua ya kuendelea kusubiri wakisema wanahitaji kuwazika watoto wao mapema ili waanze safari ya kuponya majeraha ya msiba huo.
Mchungaji Dan Parisoi ambaye ni jamaa wa marehemu Purity Naisula amesema kucheleweshwa kwa mazishi kunaongeza maumivu kwa familia ambazo tayari zimeathirika na tukio hilo.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Gilgil Stanley Langat Mutai amesema mashauriano yanaendelea kuhusu ombi la baadhi ya wazazi wanaotaka miili ya watoto wao ikabidhiwe mapema.
