KIONGOZI wa Wiper Patriotic Front, Kalonzo Musyoka, wikendi alizindua rasmi jukwaa la kuendesha kampeni zake za urais, akiahidi kubadilisha maisha ya Wakenya dhidi ya kile alichokitaja kuwa ni uongozi mbaya, ufisadi na kupanda kwa gharama ya maisha.
Uzinduzi huo ulifanyika miezi kadhaa baada ya Wiper kumuidhinisha rasmi Bw Musyoka kuwa mgombea wake wa urais.
Kuidhinishwa huko kulichukuliwa na washirika wake kama mwanzo wa kampeni zake za kuingia ikulu 2027.
Bw Musyoka atakuwa akiwania urais kwa mara ya pili baada ya kugombea mnamo 2007 na kumaliza nyuma ya marehemu Mwai Kibaki na Raila Odinga.
Bw Musyoka, katika mahojiano ya awali amewahi kusema kuwa kujiondoa tena katika kinyangányiro cha urais mnamo 2027 kungekuwa sawa na kustaafu siasa za ushindani.
Atakuwa akitumia kaulimbiu ya “Kalonzo 2027”.
Kwa mujibu wa kura ya maoni ya TIFA iliyotolewa mwezi uliopita, Bw Musyoka ndiye anayeshika nafasi ya pili kwa umaarufu miongoni mwa wanaotajwa kuwa wagombea wa urais.
Asilimia 19 ya Wakenya walimtaja kama chaguo lao kuu la urais.
William Ruto aliongoza kwa asilimia 24 huku Fred Matiang’i akifuatia kwa asilimia 14.
Akihutubia wafuasi, magavana, wabunge, wanadiplomasia, viongozi wa biashara na wanachama wa upinzani jijini Nairobi, Bw Musyoka alisema jukwaa hilo ni zaidi ya tovuti ya kampeni, akilitaja kama uzinduzi rasmi wa vuguvugu lake la “KOMBOA Kenya”.
