Waziri Msaidizi Ken Obura ametangaza kuwa hatawania ugavana wa Kisumu kupitia chama cha ODM.
Badala yake, amesema atawania kiti hicho kama mgombeaji huru katika uchaguzi mkuu ujao.
Tangazo hilo linajiri wakati ambapo wagombea tisa wanapania kupata tikiti ya ODM kuwania ugavana wa Kisumu.
Obura, ambaye kwa sasa anahudumu kama Mkuu wa Mipango katika afisi ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki, amesema hana nia ya kutumia rasilimali zake katika mchakato wa uteuzi wa chama hicho.
Amedai kuwa ODM haina demokrasia ya kutosha na kwamba hataki kupitia hali kama aliyodai kuikumbana nayo mwaka 2022.
Obura pia amesema uongozi wa ODM umewaangusha wakazi wa Kisumu tangu kuanzishwa kwa ugatuzi na kwamba ni wakati wa wapigakura kufanya maamuzi tofauti.
Miongoni mwa wanaotajwa kusaka tikiti ya ODM ni Seneta Tom Ojienda, Mbunge wa Nyakach Aduma Owuor, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga, Mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron pamoja na Naibu Gavana Mathews Owili.
