Mahakama Kuu imeagiza Wizara ya Afya kufichua ndani ya siku saba maelezo yote yanayohusiana na mpango wa kuanzisha kituo cha karantini na matibabu ya Ebola kwa raia wa Marekani nchini Kenya.
Mahakama imemtaka Waziri wa Afya, Aden Duale, kuwasilisha stakabadhi zote za makubaliano kati ya Kenya na Marekani kuhusu mpango huo, ikiwemo mikataba, mazungumzo na hati za maelewano zilizotiwa saini.
Aidha, serikali imeagizwa kueleza iwapo Bunge, serikali za kaunti na taasisi husika zilishirikishwa kabla ya uamuzi wa kuanzisha kituo hicho kufikiwa.
Katika uamuzi huo, mahakama pia imezuia serikali kuendelea na ujenzi au kuanzisha kituo chochote cha karantini au matibabu ya Ebola nchini hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.
Hatua hiyo imekuja huku maandamano yakishuhudiwa jijini Nairobi na mjini Nanyuki, ambapo wananchi na wanaharakati wamekuwa wakipinga mpango huo wakidai haukuwa na mashauriano ya kutosha ya umma.
Wakati huo huo, mashirika ya kutetea haki za binadamu na Chama cha Wanasheria nchini, LSK, yamehoji uhalali wa mpango huo, yakisema haukupitishwa na Bunge wala kufanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira na afya ya umma.
Kwa upande wake, serikali imesisitiza kuwa maandalizi dhidi ya magonjwa ya mlipuko ni sehemu ya usalama wa taifa na kwamba Kenya ina jukumu la kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika masuala ya afya.
Kesi hiyo itatajwa tena Juni 23 kwa maelekezo zaidi na kuthibitisha utekelezaji wa amri za mahakama.
