Wakulima wa Chai Walalamikia Ushuru Mpya wa Asilimia 0.8 

Wakulima wa majani chai kutoka maeneo mbalimbali nchini wameibua wasiwasi mkubwa kuhusu ushuru wa asilimia 0.8 uliopendekezwa katika Mswada wa Majani Chai, wakisema hatua hiyo itaongeza mzigo kwa wakulima na kudhoofisha sekta hiyo muhimu ya uchumi.

Akizungumza katika kaunti ya Kiambu, mwenyekiti wa kiwanda cha majani chai cha Kagwe, William Muroki Githumbi, alisema wakulima hawakuhusishwa katika utoaji wa maoni kuhusu ushuru huo, jambo alilotaja kuwa ni ukiukaji wa katiba.

Githumbi alionya kuwa iwapo mswada huo utapitishwa jinsi ulivyo, baadhi ya mawakala wanaweza kutumia mwanya huo kuchanganya majani chai ya kiwango cha chini na yale ya ubora wa juu kutoka kwa wakulima, hali ambayo inaweza kushusha thamani ya majani chai ya Kenya katika soko la kimataifa.

Aidha, alisema ushuru pamoja na matozo mbalimbali kwenye sekta ya majani chai yameendelea kuongezeka na sasa kufikia asilimia 42, hali inayowaumiza zaidi wakulima wanaotegemea zao hilo kujikimu kimaisha.

Aliwataka wabunge hasa kutoka maeneo yanayolima majani chai kusimama kidete kutetea wakulima na kuhakikisha sekta hiyo inalindwa dhidi ya kile alichokitaja kama ushuru wa kupita kiasi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *