Kiongozi wa chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ameutaja mpango wa serikali kwa serikali (G-to-G) wa uagizaji mafuta kuwa “ulaghai”, akiishutumu serikali ya Rais William Ruto, pamoja na baadhi ya wafanyabiashara kwa kuwaumiza Wakenya kupitia ongezeko la bei ya mafuta.
Akizungumza kabla ya kuondoka kuelekea United Kingdom, Gachagua alisema mzozo wa sasa wa bei ya mafuta nchini Kenya hauhusiani na bei ya mafuta duniani, akidai kuwa nchi jirani zinazonunua mafuta kutoka Mashariki ya Kati zinauza mafuta kwa bei ya chini zaidi.
Alidai kuwa faida kubwa zinazochukuliwa na baadhi ya maslahi ya kibiashara yanayohusishwa na serikali, ikiwemo Gulf Energy, ndizo zimechangia kupanda kwa bei ya mafuta nchini.
Kulingana na Gachagua, bei ya mafuta nchini Kenya bado iko juu kuliko katika mataifa jirani licha ya kutumia vyanzo sawa vya usambazaji.
Alisema kuwa petroli nchini Kenya kwa sasa inauzwa kwa shilingi 214 kwa lita, huku dizeli ikiuzwa kwa shilingi 243, akilinganisha na taifa la Uganda ambako petroli ni shilingi 88 na dizeli shilingi 181 licha ya mafuta hayo kusafirishwa kwa barabara kutoka Bandari ya Mombasa.
Pia alitaja mataifa kama Rwanda, Tanzania na Ethiopia kama mifano ya mataifa yenye bei nafuu zaidi ya mafuta kuliko nchini Kenya.
Gachagua, pia aliikosoa serikali kwa kuruhusu uingizaji wa mafuta yenye kiwango cha sulphur cha miligramu 50, akidai hatua hiyo imeathiri ubora wa mafuta nchini.
Aidha, alidai bila kutoa ushahidi kuwa faida zinazotokana na ongezeko la bei ya mafuta zilitumika katika ununuzi wa mali za Tullow Oil huko Turkana.
Kauli zake zinajiri baada ya Energy and Petroleum Regulatory Authority (EPRA) kuongeza bei ya Super Petrol na Diesel kwa shilingi 16.65 na shilingi 46.29 kwa lita mtawalia katika mapitio yake ya hivi karibuni.
Marekebisho hayo yamefanya bei ya Super Petrol jijini Nairobi kufikia shilingi 214.25 kwa lita huku Diesel ikiuzwa kwa shilingi 242.92 kwa lita.
