Kiongozi wa People’s Liberation Party, Martha Karua, ameilinganisha hali ya sasa ya uchumi nchini Kenya na changamoto zilizoshuhudiwa wakati wa utawala wa hayati Daniel arap Moi, akisema taifa bado limekwama katika mzunguko wa gharama kubwa ya maisha, utawala mbovu na matarajio yasiyotimizwa.
Kupitia ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Karua alikumbuka hali ya mwezi Juni mwaka 1997 wakati wa utawala wa Moi, akisema kuwa hata wakati huo bei ya mafuta pamoja na gharama ya maisha zilikuwa changamoto kubwa kwa Wakenya.
Karua, alisema licha ya taifa la Kenya kuwa na uwezo mkubwa wa kiuchumi,taifa hili bado halijafanikiwa kujinasua kutoka katika changamoto za mara kwa mara za kiutawala.
Aidha, aliwataka Wakenya kuungana na kufanya mabadiliko ya uongozi kwa kuwachagua viongozi wenye uwezo wa kushughulikia changamoto za mfumo wa utawala.
Kauli zake zinakuja baada ya EPRA kuongeza bei ya Super Petrol na Diesel kwa shilingi 16.65 na shilingi 46.29 kwa lita mtawalia.
Bei mpya zimeifanya Super Petrol Nairobi kuuzwa kwa shilingi 214.25 kwa lita huku Diesel ikifikia shilingi 242.92 kwa lita.
Kwa kulinganisha, wastani wa bei ya mafuta mwaka 1997 ulikuwa shilingi.34.55 kwa Super Petrol, shilingi 27.30 kwa Diesel na shilingi 20.85 kwa mafuta ya taa, hali inayoonyesha ongezeko kubwa la gharama za bidhaa za petroli kwa kipindi cha miaka mingi iliyopita.
