Kiongozi wa Orange Democratic Movement (ODM), Oburu Oginga, ametetea ushirikiano wa chama hicho na serikali ya Kenya Kwanza akisema umeleta manufaa ya kisiasa na kiuchumi kwa wafuasi wa chama hicho pamoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa mkutano wa wadau uliofanyika Nyakach siku ya Ijumaa, mwanasiasa huyo mkongwe alisema uamuzi wa ODM kufanya kazi na serikali jumuishi umewezesha chama hicho kushawishi maamuzi muhimu ya kitaifa kutoka ndani ya mifumo ya serikali.
Mkutano huo uliowaleta pamoja wadau wa chama ulilenga kuweka mikakati ya pamoja ya ODM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Oburu aliwahimiza wanachama wa chama hicho kudumisha umoja na kuunga mkono maamuzi ya uongozi wa chama, akirejelea tofauti zilizopo kati ya makundi ya Linda Mwananchi na Linda Ground.
Kiongozi huyo wa ODM pia, alifichua kuwa chama hicho kinaimarisha ushirikiano wa mashinani kwa kuwawezesha viongozi wa maeneo na wabunge wa mabunge ya kaunti ili kuimarisha mawasiliano kati ya uongozi na wananchi.
Kulingana na Oburu, mkakati huo unalenga kuboresha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya chama na wananchi huku ukidumisha uungwaji mkono katika ngazi ya mashinani.
Wakati huo huo, Oburu alitangaza kuwa ODM imeanzisha kampeni kali ya kuandikisha wanachama wapya ikiwalenga vijana na wanawake kupitia mifumo ya kidijitali.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa ODM na serikali iliyoko madarakani unalenga kulinda maslahi ya wafuasi wake na kuhakikisha ushirikishwaji katika uongozi wa kitaifa.
