Skip to content

Kuccps yafungua upya awamu ya pili ya maombi ya vyuo vikuu

Shirika la KUCCPS limefungua tena awamu ya pili ya maombi ya kujiunga na vyuo vikuu kwa watahiniwa wa KCSE 2025.

Wanafunzi sasa wana nafasi nyingine ya kubadilisha kozi walizochagua au kutuma maombi mapya.

Kupitia taarifa iliyotolewa Mei 16, 2026, KUCCPS ilisema mfumo wa maombi utafunguliwa hadi Mei 22, 2026. Awamu ya kwanza ya maombi ilifungwa Mei 6.

Mkurugenzi Mkuu wa KUCCPS, Agnes Mercy Wahome, alisema wanafunzi waliopata nafasi za muda katika kozi za shahada tayari wamepokea ujumbe mfupi na taarifa kupitia mfumo wa KUCCPS. Wale ambao hawakupata nafasi wameombwa kurekebisha uchaguzi wao wa kozi.

KUCCPS pia, ilisema kuwa wanafunzi 212,510 waliopata alama ya C+ na kuendelea katika KCSE 2025 tayari wameomba kozi mbalimbali.

Hii ni asilimia 79.1 ya wanafunzi wote 268,714 waliohitimu kujiunga na vyuo vikuu.

Baadhi ya kozi zinazohitajika sana kama Udaktari, Uuguzi, Famasi na Uhandisi tayari zimejaa kutokana na idadi kubwa ya waombaji. Kwa sababu hiyo, kozi hizo zimeondolewa kwenye mfumo wa maombi kwa sasa.

Wakati huo huo, maombi ya kujiunga na vyuo vya TVET, KMTC na Kenya Utalii College bado yanaendelea hadi nafasi zote zijazwe.

Katika KMTC, baadhi ya kozi zinazopatikana ni Afya ya Jamii, Sayansi ya Mochari, Teknolojia ya Rekodi za Afya, Uhandisi wa Tiba, Sayansi ya Maabara, Fiziotherapia na Afya ya Umma. Pia kuna kozi nane za cheti zinazotolewa.

Hata hivyo, KUCCPS imesema kozi za Uuguzi, Tiba ya Kliniki na Famasi hazipatikani kwa sasa na zitafunguliwa tena mwezi Septemba.

Katika Kenya Utalii College, kozi zinazopatikana ni pamoja na Usimamizi wa Housekeeping na Laundry, Front Office pamoja na Housekeeping Operations.

Kozi hizi ziko wazi kwa wanafunzi waliofanya KCSE kuanzia mwaka 2000 hadi 2025.

Ili kusaidia wanafunzi kufanya maombi, KUCCPS imepeleka maafisa wa ushauri wa taaluma katika vyuo 23 za KMTC nchini kote.

Pia huduma za usaidizi zinapatikana katika vituo 59 vya Huduma Centres nchini kupitia ushirikiano na Huduma Kenya Secretariat.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *