Baadhi ya wafanyakazi katika ofisi ya naibu wa rais nchini watarajiwa kujiuzulu huku maafisa wakuu katika ofisi za umma wakionya kuwa wengi wa wafanyakazi huenda wakajiuzulu kabla ya uchaguzi mkuu mwaka 2027, hali iliyosababisha kuongeza kwa mgao wa shilingi milioni 95.4 kwa ajili ya malipo ya watumishi hao wakati watakapoondoka kazini.
Suala hilo lilijiri wakati wa uwasilishaji wa makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 mbele ya kamati ya bunge ya utawala na usalama wa ndani, inayoongozwa na mbunge wa Narok Magharibi, Gabriel Tongoyo.
Katibu wa utawala, Moses Mbaruku, aliiambia kamati hiyo kuwa kuongezeka kwa matamanio ya kisiasa miongoni mwa wafanyakazi kumesababisha hofu ya ongezeko la kuondoka kwa wafanyakazi katika ofisi hiyo.
Aliiambia kamati hiyo kuwa wafanyakazi wengi wako kwenye mikataba ya ajira na idadi kubwa yao imeeleza nia ya kuacha utumishi wa umma ili kugombea nafasi za kisiasa au kushiriki katika shughuli za uhamasishaji wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.
Ofisi ya naibu wa rais hapo awali ilikuwa imetengewa shilingi bilioni 3.581 chini ya viwango vya taarifa ya sera ya bajeti (BPS), ikijumuisha shilingi bilioni 3.481 kwa matumizi ya kawaida na shilingi milioni 100 kwa matumizi ya maendeleo.
Hata hivyo, makadirio yaliyorekebishwa yaliongeza bajeti hiyo hadi shilingi bilioni 3.676 yakionyesha ongezeko la shilingi milioni 95.4 katika matumizi ya kawaida, hasa kwa mishahara na malipo ya kutamatisha kandarasi kwa wafanyakazi wanaoondoka.
Mwenyekiti wa kamati, Tongoyo, aliomba ufafanuzi kuhusu tofauti hiyo, akiuliza kama marekebisho hayo yalihusiana na mishahara ya wafanyakazi au maeneo mengine ya matumizi.
Mbaruku alitetea takwimu hizo zilizorekebishwa, akisema utekelezaji wa bajeti katika ofisi hiyo umeendelea vizuri.
