Rais William Ruto alifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Chanjo (IVI), Jerome Kim, katika Ikulu ya Nairobi.
Rais Ruto alithibitisha tena dhamira ya Kenya kuendelea kushirikiana katika utafiti na maendeleo ya chanjo, majaribio ya kitabibu, ushirikiano wa utengenezaji wa chanjo, kuimarisha mifumo ya udhibiti pamoja na maendeleo ya wafanyakazi.
Taasisi hiyo inafungua Ofisi mpya ya Nchi na Mradi nchini Kenya, hatua inayotajwa kuwa muhimu katika juhudi za kuendeleza utafiti na maendeleo ya chanjo barani Afrika.
Makubaliano hayo yanathibitisha rasmi uwepo wa IVI nchini Kenya, yakionyesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha utafiti na maendeleo ya chanjo, tafiti za maabara na mashinani, ubunifu wa bidhaa pamoja na kujenga uwezo kupitia mafunzo ya wafanyakazi na uhamishaji wa teknolojia.
Waziri Mkuu wa zamani ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Diaspora, Musalia Mudavadi, alisema kuanzishwa kwa Ofisi ya IVI nchini Kenya, kunaonyesha dhamira ya pamoja ya kuimarisha mifumo ya afya, kuendeleza utafiti na maendeleo pamoja na kuhimiza utengenezaji wa bidhaa za afya nchini Kenya na barani Afrika kwa ujumla.
Mudavadi alitangaza kuwa IVI itafanya kazi kwa karibu na taasisi za kitaaluma na za utafiti nchini ikiwemo Taasisi ya Utafiti wa Matibabu Kenya (KEMRI), Kenya Biovax Institute na Bodi ya Famasi na Sumu.
Makubaliano ya nchi mwenyeji ya kuanzisha Ofisi ya IVI Kenya na Mradi wa AVEC Africa yalitiwa saini na Musalia Mudavadi pamoja na mkuu wa IVI mbele ya Rais William Ruto.
