Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ameongeza wito wa kumchagua tena Rais William Ruto akisema eneo la Mlima Kenya linafaa kuheshimu ahadi zake za kisiasa za awali.
Waiguru alisema eneo hilo lina hatari ya kutengwa kisiasa kwa kumsaliti Rais Ruto kwa kushindwa kutimiza makubaliano ya kisiasa yaliyofanywa wakati wa uongozi wa aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta.
Aliwakumbusha wakazi wa eneo hilo kuhusu ahadi iliyotolewa waziwazi ya kumuunga mkono Uhuru Kenyatta, kwa mihula miwili na baadaye kumuunga mkono Ruto kwa miaka kumi, akisema kutimiza ahadi hiyo kutalipa eneo hilo heshima kitaifa.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumkaribisha na kumshukuru Mwakilishi wa Wanawake wa Nyeri Rahab Mukami kufuatia kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa Caucus ya Wanawake katika Bunge la Pan Afrika, Waiguru alisema eneo hilo linapaswa kubaki thabiti na la kuaminika kisiasa kwa kutimiza ahadi zilizotolewa wakati wa uchaguzi uliopita.
Wakati huo huo, gavana huyo alijaribu, kutuliza mvutano wa kisiasa katika eneo hilo kufuatia kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, hatua ambayo imeripotiwa kuzua kutoridhika miongoni mwa baadhi ya wapiga kura wa Mlima Kenya.
Waiguru aliomba radhi kwa wakazi wa eneo hilo, akitambua hali ya sintofahamu iliyosababishwa na tukio hilo na kuwataka kudumisha umoja kuelekea mbele.
Kauli zake ziliungwa mkono na Gavana wa Nakuru Susan Kihika ambaye alisisitiza umuhimu wa kuimarisha uungwaji mkono kwa Rais Ruto.
Kihika alisema kuwa kumchagua tena Rais Ruto kutasaidia kulinda maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya wanaoishi na kufanya biashara sehemu mbalimbali nchini, hivyo kuimarisha hisia za kujumuishwa na usalama ndani ya taifa.
Seneta wa kuteuliwa Veronica Maina pia ,aliwataka wakazi wa eneo hilo kumuunga mkono Rais, akieleza kile alichokitaja kuwa mafanikio ya maendeleo chini ya utawala wake.
Alitaja miradi mikubwa inayoendelea na iliyokamilika katika eneo hilo kama ushahidi wa dhamira ya Serikali ya kuboresha maisha ya wananchi.
