Kenya na Urusi zinajizatiti kuimarisha ushirikiano baina yao katika sekta za elimu, biashara, nishati na utamaduni, huku uhusiano wa nchi hizi mbili ukiendelea kuimarika.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kitaifa ya Urusi Jijini Nairobi, balozi wa Urusi nchini Kenya Vsevolod Tkachenko, alisema nchi hizi mbili zimepiga hatua ya kumezewa mate katika siasa, uchumi na ushirikiano wa utamaduni kwa muda mrefu.
Balozi huyo alitaja Kenya kuwa mojawepo wa chumi bora zaidi barani Afrika na mshirika muhimu wa Urusi katika kanda ya Afrika Mashariki.
Aidha, alitaja ziara ya Jijini Moscow ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi, kuwa hatua muhimu ya kufungua fursa mpya za mashauriano ya kiuchumi na ushirikiano thabiti.
Kulingana na balozi huyo, ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili ulifikia dola milioni 600 mwaka 2025, ukipigwa jeki na bidhaa zinazoingizwa hapa nchini kutoka Russia za ngano na mbolea, huku Kenya ikiuza nchini Russia maua, Majani Chai na Kahawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa maswala ya kidiplomasia katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya Josphat Maikara, aliyemwakilisha Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi katika maadhimisho hayo, alisema Kenya imejitolea vilivyo kupanua ushirikiano wake na Russia katika sekta mbali mbali.
Maadhimisho hayo yaliwaleta pamoja wanadiplomasia, maafisa wa serikali, viongozi wa kibiashara, wasomi, wanahabari raia wa Urusi na marafiki wa Urusi.
