William Ruto amesema Kenya inaendelea kufanya mageuzi ya mfumo wa elimu ili kuhakikisha wanafunzi wanaendana na soko la ajira duniani linalobadilika kwa kasi, hasa katika sekta ya teknolojia.
Rais alisema mfumo wa elimu wa Competency-Based Education (CBE) una mwelekeo wa vitendo zaidi na unalenga kukuza ujuzi, maarifa na uwezo wa wanafunzi.
Alikuwa akizungumza katika kongamano la vijana lililoandaliwa katika chuo kikuu cha Nairobi katika ambalo lilihudhuriwa pia na rais wa Ufaranza Emmanuel Macron ikiwa ni mojawapo ya sehemu ya shughuli za mkutano wa Africa Forward Summit.
Ruto alisema mfumo wa zamani wa elimu ulikuwa ukijikita zaidi katika kukariri na kurudia yaliyohifadhiwa akilini. Alieleza kuwa mageuzi hayo yanalenga kutoa maarifa yanayoendana na mahitaji ya sasa katika kutoa ajira.
Aidha, alisema mfumo wa CBE unatilia maanani zaidi masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), ambayo ni msingi wa ubunifu na maendeleo ya teknolojia.
Kuhusu teknolojia, Rais alisema serikali imeweka kilomita 30,000 za nyaya za fibre optic ili kupanua miundombinu ya kidijitali na kuunda nafasi kwa wabunifu, wavumbuzi na biashara mbalimbali.
Rais aliongeza kuwa uwekezaji huu utaifanya Kenya kuwa kitovu cha ubunifu kwani utavutia wawekezaji kwa kujenga mfumo madhubuti wa teknolojia huku akieleza kuwa Kenya inapiga hatua katika utengenezaji wa vifaa vya kidijitali kama simu na kompyuta.
Kwa upande wake, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliipongeza Kenya kwa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kidijitali. Alihimiza nchi za Afrika kuunda mazingira mazuri ya ubunifu na kushirikiana kujenga uwezo wa matumizi ya AI pamoja na mifumo ya malipo ya kuvuka mipaka.
Macron alisema Afrika inapaswa kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia nishati jadidifu na nyuklia ili kusaidia vituo vya data na miundombinu mingine ya kidijitali.
Mjadala huo ulikuwa sehemu ya kongamano la Africa Forward Summit jijini Nairobi lililowaleta pamoja wakuu wa nchi 30 na maelfu ya washiriki ikiwa na mara ya kwanza kwa mkutano huo kufanyika barani Afrika.
