Mvutano umeibuka kuhusu mpango wa upanuzi wa uwanja wa ndege kaunti ya Wajir huku waamiliki wa ardhi walioathirika wakitishia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mamlaka ya viwanja vya ndege pamoja na serikali ya kaunti hiyo.
Wakazi hao wanadai kuna unyakuzi wa ardhi kinyuma cha sheria na kuwa wametengwa katika vikao muhimu vya mashauriano.
Zaidi ya familia 400 zinaripotiwa kuathirika huku wakiishutumu mamlaka hiyo kwa kukosa kushirikisha umma na kushindwa kutoa fidia kabla ya kutenga ardhi hiyo kwa ajili ya upanuzi huo.
Aidha kupitia kwa wakili wao Jamal Abdikadir wakaazi hao wanadai walitengwa katika mikutano yao iliyofanyika mjini Wajir mwezi uliopita kujadili ununuzi wa ardhi binafsi unaopakana na uwanja wa ndege.
Upananuzi wa uwanja huo unatarajiwa kuimarisha zaidi sekta ya usafiri katika eneo hilo pamoja na kuimarisha biashara huku serikali ya kitaifa ikitoa hakikisho kwamba wale watakaoathirika watafidiwa.
