Vijana na wahudumu wa bodaboda mjini Marsabit mapema Jumatatu waliungana na wakenya wengine kushiriki maandamano ya kulalamikia ongezeko la bei ya mafuta.
Mandamano hayo yalikatiza shughuli za biashara, huku baadhi ya maduka yakisalia kufungwa mapema Jumatatu
Maafisa wa polisi walilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya wandamanaji waliokuwa wakiteketeza magurudumu ya magari na kuziba barabara kuu ya Marsabit-Moyale kwa kutumia mawe.
Wandamanaji hao waliwaeleza wanahabari kuwa bei ghali ya mafuta imesababisha ongezeko la gharama ya maisha huku wakilalamikia hasara kubwa wanayopata kutokana na biashara ya uchukuzi.
Wahudumu hao pamoja na wakaazi wa Marsabit sasa wameitaka serikali ya rais William Ruto kupunguza bei ya mafuta wakihoji kuwa wanaoumia zaidi ni wananchi wa kawaida.
Jumatatu mafuta ya Dizeli mjini Marsabit yalikuwa yanauzwa kwa shilingi 256.10 huku petroli ikiuzwa kwa shilingi 226.50
