Skip to content

Bunge la seneti lapendekeza sheria ya kuzikinga serikali za kaunti kutokana na upungu wa fedha

Kamati ya Seneti kuhusu fedha na bajeti imewasilisha mapendekezo ya marekebisho ya muswada wa ugavi wa mapato wa mwaka 2026 ambayo yanaitaka serikali ya kitaifa kugharamia peke yake upungufu wowote wa mapato utakaojitokeza katika mwaka wa kifedha wa 2026/2027.

Marekebisho hayo, yaliyoorodheshwa katika ajenda ya Seneti kabla ya kikao cha Jumanne, yanapendekeza kifungu kipya kinachoeleza kuwa mgao wa fedha kwa kaunti hautapunguzwa iwapo mapato yatakayokusanywa kitaifa yatakuwa chini ya makadirio yaliyowekwa.

Aidha, marekebisho hayo yanaipa serikali ya kitaifa haki ya kipekee ya kutumia mapato yoyote ya ziada yatakayozidi makadirio, huku fedha hizo zikielekezwa katika kupunguza deni la taifa au kupunguza ukopaji.

Kamati hiyo pia imependekeza mfumo mpya wa ugavi wa mapato ambao utaipa serikali za kaunti jumla ya shilingi bilioni 454.74 kama mgao wa usawa, sawa na asilimia 22.2 ya mapato yaliyokaguliwa ya mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

Wakati huo huo, serikali ya kitaifa itabaki na shilingi trilioni 2.437 kutoka kwa jumla ya mapato yanayoweza kugawanywa ya shilingi trilioni 2.902.

Mfuko wa usawazishaji (Equalisation Fund) utapokea shilingi bilioni 10.25.

Marekebisho hayo yanatarajiwa kuibua majadiliano katika mazungumzo yanayoendelea kati ya seneti, bunge la kitaifa na serikali za kaunti kuhusu mgao wa mapato ya kitaifa, hasa wakati ambapo kuna shinikizo kubwa la kifedha na wasiwasi kuhusu kuendelea kuongezeka kwa deni la umma.

Maseneta wanatarajiwa kujadili mapendekezo hayo wakati wa kamati ya bunge lote siku ya Jumanne.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *