Mwaura: Wakenya wasome mswada wa fedha 2026

Serikali imewahakikishia Wakenya kuwa mswada wa Fedha mwaka 2026 haujajumuisha baadhi ya ushuru unaodaiwa kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, ikisema taarifa hizo ni za kupotosha na zenye nia ya kuzua hofu miongoni mwa wananchi.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano, msemaji wa serikali Isaac Mwaura alisema kuwa madai kuhusu ushuru mpya kwa nguo kuukuu maarufu kama “mitumba”, simu za rununu, malipo ya mtandaoni pamoja na nyongeza ya ushuru kwa nyumba za kukodisha si ya kweli,kwani baadhi ya mapendekezo hayo yaliondolewa kabla ya mswada huo kuchapishwa rasmi na hazina kuu.

Mwaura alieleza kuwa serikali imekuwa ikisikiliza maoni ya wananchi pamoja na wadau mbalimbali kuhusu baadhi ya mapendekezo yaliyokuwa yameibua mjadala mkali, jambo lililopelekea kufanyiwa marekebisho kwa vipengele kadhaa vya mswada huo kabla ya kuwasilishwa rasmi bungeni.

Alifafanua kuwa pendekezo la kuongeza ushuru wa mapato ya nyumba za kukodisha kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 10 liliondolewa, sawa na pendekezo la ushuru kwa bidhaa za mitumba ambalo lilikuwa limezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa wafanyabiashara na wananchi wa kipato cha chini.

Kwa mujibu wa Mwaura, baadhi ya taarifa zinazosambazwa mtandaoni zimekuwa zikitoa taswira isiyo sahihi kuhusu yaliyomo katika mswada wa Fedha mwaka 2026, hali ambayo alisema inaweza kuzua hisia tofauti kuhusu hali ya uchumi nchini.

Aidha aliwataka wananchi kuusoma mswada huo moja kwa moja kupitia vyanzo rasmi vya serikali badala ya kutegemea taarifa zisizothibitishwa zinazochapishwa kwenye mitandao ya kijamii.

Msemaji wa serikali pia, alitetea mswada huo akisema serikali imeweka mikakati ya kupunguza mzigo wa gharama ya maisha kwa wananchi kupitia hatua mbalimbali ikiwemo kupunguza ushuru kwa baadhi ya bidhaa za matumizi ya nyumbani pamoja na kuimarisha sekta muhimu za kiuchumi ili kusaidia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kauli hiyo ya serikali, inajiri wakati ambapo kumekuwa na mijadala mikubwa mitandaoni kuhusu mapendekezo yaliyomo kwenye mswada wa Fedha mwaka 2026, huku baadhi ya viongozi wa kisiasa na wananchi wakieleza wasiwasi wao kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa ushuru katika baadhi ya sekta nchini. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *