Anne Waiguru ametetea uamuzi wake wa kuendelea kumuunga mkono Rais William Ruto akisema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha Kaunti ya Kirinyaga inanufaika zaidi kimaendeleo kutoka serikali kuu.
Akizungumza mjini Wang’uru wakati wa uzinduzi wa mradi wa ukarabati na upanuzi wa maji wa Mwea, Waiguru alisema hakuna serikali ya kaunti inayoweza kufanikisha miradi mikubwa bila kushirikiana na serikali ya kitaifa.
Gavana huyo alisema ameamua “kuwa wa kimkakati” kwa kubaki upande wa serikali ili kupata rasilimali zaidi kwa wananchi wake. Pia alikosoa baadhi ya viongozi wa upinzani akisema wanaendesha siasa za maneno matupu bila rekodi ya maendeleo.
Kauli hiyo ilijiri baada ya aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza pamoja na aliyekuwa Mbunge wa wanawake wa Kirinyaga Wangui Ngirici kumshambulia kisiasa mwishoni mwa wiki wakimtuhumu kwa usimamizi mbaya wa kaunti.
Waiguru pia alizungumzia kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua akisema hakuhusika na mchakato huo kwani hakuwa sehemu ya Seneti wala Bunge la Kitaifa.
Aidha, aliwataka wakazi wa Kirinyaga kuzingatia siasa za maendeleo na kuwapuuza viongozi wanaotoa ahadi zisizo na msingi ambazo zinaweza kuhatarisha miradi inayoendelea kutekelezwa katika kaunti hiyo.
