Mfumo mpya wa Kuccps kubadilisha ufadhili wa vyuo vikuu

Kenya inajiandaa kwa mabadiliko makubwa katika mfumo wa ufadhili wa vyuo vikuu huku taifa likielekea katika utekelezaji wa mfumo wa elimu wa Competency-Based Education (CBE).

Akizungumza katika mahojiano, mkurugenzi mkuu wa KUCCPS Dkt. Agnes Mercy Wahome alisema kuwa mfumo mpya wa udahili utaanzisha vigezo vipya vya upangaji wa wanafunzi vinavyoendana na mfumo wa tathmini wa CBE.

Alieleza kuwa mfumo huo mpya utazingatia uwezo na umahiri wa mwanafunzi pamoja na viwango vya utendaji kama vile “kuzidi matarajio,” huku mashirika ya kitaaluma yakipewa jukumu la kubainisha masomo yanayohitajika kwa taaluma mbalimbali.

Dkt. Wahome pia, alisema uwajibikaji katika udahili wa vyuo utaimarishwa kwa kuvitaka vyuo vikuu kueleza wazi idadi ya wanafunzi wanaoweza kupokea kabla ya mchakato wa upangaji kuanza.

Aidha, vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zitatakiwa kuwasilisha idadi kamili ya wanafunzi wanaoweza kudahiliwa katika kila kozi ili kuhakikisha kuwa kuna miundombinu, wahadhiri na rasilimali nyingine za kutosha.

Alisisitiza kuwa serikali imejizatiti kuhakikisha haki na usawa katika udahili wa wanafunzi kwa kuendelea kutumia mfumo wa merit katika upangaji wa wanafunzi.

Kwa mujibu wake, mara tu Baraza la Mitihani la Kenya (KNEC) linapotangaza matokeo ya KCSE, mfumo wa kidijitali wa KUCCPS hupanga wanafunzi kuanzia waliopata alama za juu hadi za chini kulingana na nafasi zilizopo katika kila kozi.

Dkt. Wahome alisema ushindani huwa mkubwa kwa sababu wanafunzi wengi hushindania nafasi chache zilizopo, hali inayofanya mwanafunzi anayechukua nafasi ya mwisho kuwa ndiye anayebainisha kiwango cha mwisho cha udahili.

Pia alibainisha kuwa vyuo vikuu vimewekeza pakubwa katika sekta ya elimu ya juu na kuongeza nafasi za udahili kwa wanafunzi wapya.

Aliongeza kuwa mfumo wa CBE, utapunguza ushindani usio wa lazima kwa kuwa wanafunzi wataweza kujikita mapema katika nyanja kama STEM, sanaa, michezo na masomo ya kijamii, hivyo kupanua fursa kwa kila mwanafunzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *