Skip to content

Maandalizi ya siku kuu ya madaraka wajir yafikia asilimia 84

Maandalizi ya sherehe za kitaifa za siku ya Madaraka mwaka huu, zitakazofanyika katika Kaunti ya Wajir sasa yamekamilika kwa asilimia 84, huku Serikali ikiwa na imani kuwa kazi zote muhimu zitakuwa zimekamilika mapema kabla ya hafla hiyo tarehe mosi mwezi wa Juni 2026.

Katibu Mkuu wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, Raymond Omollo, alieleza kuridhishwa kwa Serikali na maendeleo hayo baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa maeneo muhimu na kazi zinazoendelea mjini Wajir.

Omollo, alisema kuwa sehemu kubwa ya kazi zilizobaki zinatarajiwa kukamilika kati ya tarehe 20 na 25 mwezi huu wa Mei, hali itakayotoa muda wa kutosha kwa majaribio ya mwisho, mazoezi na shughuli za uratibu kabla ya siku ya sherehe.

Ukaguzi huo ulijumuisha eneo kuu la sherehe, miradi ya miundombinu, mazoezi ya gwaride pamoja na vifaa vingine vinavyoandaliwa kwa ajili ya kuandaa hafla hiyo ya kitaifa.

Mazoezi na shughuli za uratibu tayari zimeanza, ikiwemo mafunzo ya gwaride yanayohusisha vikosi mbalimbali vya usalama na timu za sherehe zitakazoshiriki siku hiyo.

Kama sehemu ya maandalizi, Serikali itaandaa wiki maalum kuanzia tarehe 25 hadi 31 Mei 2026 katika Shule ya Msingi ya Wagberi.

Wiki hiyo itazingatia elimu, ujuzi na mustakabali, mada inayolingana na maadhimisho ya siku kuu ya Madaraka ya mwaka huu.

Rais William Ruto pia, ataandaa chakula cha kitaifa kwa wageni waalikwa.

PS Omollo alisisitiza kuwa kuandaliwa kwa kwa siku hiyo mjini Wajir, kunaonyesha dhamira ya Serikali ya maendeleo jumuishi, mshikamano wa kitaifa na usambazaji sawa wa hafla za kitaifa katika maeneo yote ya nchi.

Pia aliwataka wananchi kuzingatia muda wa ratiba ya shughuli hizo, akibainisha kuwa ratiba ya siku ya Madaraka imepangwa kwa kuzingatia sala za adhuhuri zinazotekelezwa katika eneo hilo.

Serikali imewaalika Wakenya kutoka sehemu mbalimbali za nchi kuungana na wakazi wa Wajir katika kuadhimisha siku ya Madaraka ya mwaka huu.

PS Omollo, ameandamana na Katibu Mkuu wa Utamaduni na Urithi, Ummi Bashir, Gavana wa Kaunti ya Wajir Ahmed Abdullahi pamoja na maafisa kutoka wizara, idara na mashirika mbalimbali yanayoratibu sherehe hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *