Kongamano la Roots Party jijini Nairobi

Kingozi wa Roots Party profesa George Wajackoyah aliwaongoza wanachama wake kwenye kongamano la kitaifa la wajumbe (NDC) siku ya Jumamosi Mei 23, 2026, jijini Nairobi huku likiwavutia wajumbe kutoka kote nchini.

Kwenye kongamano hilo kiongozi huyo aliweka wazi azma yake ya kuwani kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu ujao mwaka wa 2027 huku wajumbe wakitumia nafasi hiyo kupanga mikakati ya jinsi watakavyoshiri uchaguzi huo.

Wajumbe waliohudhuria walimuunga mkono Prof. Wajackoyah kuendelea kuwa kiongozi wa chama hicho na kusisitiza kuwa wataangazia mabadiliko ya kiuchumi na kuhamasisha wakenya mashinani.

Akiwahutubia wajumbe kinara wa Roots Party alisema kuwa watazingatia zaidi mifumo ya kimataifa hasa katika kuboresha uchumi kama vile, Canada, bara la Ulaya na kwengineko na kusema wanalenga maono ya muda mrefu badala ya miungano ya muda mfupi.

Naye katibu wa chama hicho Cecil Miller aliwaeleza wajumbe hatua zilizopigwa na Roots Party tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2022 na kutoa wito wa hamasa zaidi na kusisitiza haja ya nidhamu, kuzingatia sera na kuepuka mashirikiano ya muda mfupi.

Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi ambaye alihudhuria kongamano hilo alisema kuwa Prof. Wajackoyah ni mmoja wa viongozi wachache wanaozungumza kwa ujasiri kuhusu masuala yanayohusu Wakenya wa kawaida na kutetea mageuzi.

Kauli za viongozi hao zinajiri wakati vyama mbali mbali vya kisiasa nchini vikiendelea na mikakati ya kujianda kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao kwa lengo la kupata ushindi.