Aliyekuwa Jaji Mkuu, Bw. David Maraga, ameonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la watoto wanaopotea, kutekwa nyara na kusafirishwa kiharamu nchini Kenya, akisema hali hiyo imefikia kiwango cha kutisha kinachohitaji hatua za haraka za kitaifa.
Katika taarifa yake, Maraga alinukuu takwimu kutoka mfumo wa Child Protection Information Management System (ICPIMS) zikionyesha kuwa kati ya Januari 2025 hadi Machi 2026, zaidi ya visa 10,500 vya ulinzi wa watoto viliripotiwa. Kati ya hivyo, 1,952 vilihusisha utekaji nyara, 1,636 watoto waliopotea, pamoja na matukio mengine ya biashara haramu ya watoto.
Alibainisha kuwa hali hiyo inaonyesha ongezeko kubwa ukilinganisha na mwaka 2024, ambapo zaidi ya watoto 8,800 waliripotiwa kupotea, sawa na wastani wa watoto 17 hadi 18 kila siku.
Maraga pia alisema visa vya watoto kupotea vinaongezeka kila mwaka, akitaja takwimu za 6,841 katika kipindi cha awali, 7,058 mwaka 2023/2024, na zaidi ya 8,800 mwaka 2024.
Alieleza pia wasiwasi wake kuhusu kiwango cha chini cha urejeshaji wa watoto kwa familia zao, akibainisha kuwa mwaka 2022/2023 ni asilimia 1.2 pekee ya karibu visa 7,000 vilivyoripotiwa vilifanikiwa kuunganishwa tena na familia zao.
Ametaka vyombo vya usalama, ikiwemo DCI, Wizara ya Jinsia, Utamaduni na Huduma kwa Watoto pamoja na serikali za kaunti, kushughulikia visa hivyo kwa uzito sawa na uhalifu mwingine mkubwa. Amehimiza ushirikiano wa karibu, uchunguzi wa haraka na mifumo madhubuti ya uwajibikaji.
Maraga ametaja Nairobi, Nakuru, Kakamega, Homa Bay na Kiambu kuwa maeneo hatarishi yanayohitaji operesheni maalum za kiusalama.
Pia ameonya kuhusu ongezeko la unyanyasaji wa watoto mtandaoni, akibainisha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 18 hutumia mtandao mara kwa mara, hali inayowaweka katika hatari ya kudanganywa na kuingizwa kwenye mitandao ya uhalifu.
Aidha, amesisitiza kuimarishwa kwa huduma ya Child Helpline 116 kupitia kuongeza wafanyakazi, kuongeza uelewa wa umma na kuboresha kasi ya kujibu taarifa za dharura.
Pia amegusia watoto wenye ulemavu, akibainisha kuwa baadhi ya visa vilivyoripotiwa mwaka 2025 vilihusisha watoto wenye tawahudi, kifafa na changamoto za kusikia au kuzungumza, ambao wanahitaji ulinzi maalum.
Maraga amehitimisha kwa kuitaka serikali kuongeza uwekezaji katika mifumo ya ulinzi wa watoto na kuimarisha msaada kwa mashirika ya kiraia yanayosaidia kutafuta watoto waliopotea na kusaidia familia zilizoathirika.
