Viongozi kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya wameongeza shinikizo wakitaka eneo hilo kupewa nafasi ya Naibu Rais katika mikakati ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 chini ya serikali ya Kenya Kwanza.
Wito huo ulijitokeza wakati wa mkutano mkubwa wa viongozi uliofanyika Naivasha na kuhudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, magavana pamoja na zaidi ya wabunge 28 kutoka eneo la Magharibi.
Viongozi hao walisema eneo hilo lina idadi kubwa ya wapigakura na limeendelea kuunga mkono serikali ya Rais William Ruto, hivyo linastahili kupewa nafasi kubwa zaidi katika uongozi wa taifa.
Baada ya mkutano huo uliofanyika Lake Naivasha Resort, viongozi hao waliwaambia wanahabari kuwa Magharibi mwa Kenya kwa muda mrefu imekuwa ikiunga mkono tawala mbalimbali lakini bado haijapata uwakilishi wa kutosha katika nafasi za juu serikalini.
Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka alisema kuwa viongozi wa eneo hilo wameungana kuhakikisha Magharibi inapata nafasi kubwa zaidi katika siasa za kitaifa.
