Rais William Ruto, ameagiza Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) kuruhusu wahudumu wa matatu kuendelea kutumia michoro ya graffiti na sanaa kwenye magari ya uchukuzi wa umma.
Akizungumza kutoka Ikulu ya Mombasa, Rais alisema serikali itahakikisha mazingira mazuri kwa waendeshaji wa matatu kuendelea kuonyesha ubunifu na sanaa kwenye magari yao huku wakizingatia usalama wa barabarani na kuheshimu watumiaji wengine wa barabara.
Agizo hilo linajiri miezi kadhaa baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi iliyokuwa ikipinga maagizo ya NTSA kuhusu graffiti, vioo vya tinted na taa za mapambo kwenye matatu.
Katika kesi hiyo, waliowasilisha ombi walidai kuwa masharti hayo yalikuwa yanatishia utamaduni wa kipekee wa matatu nchini Kenya, lakini mahakama iliamua kuwa NTSA ilikuwa ndani ya mamlaka yake katika kuimarisha usalama barabarani.
Kiongozi wa taifa,alitoa matamshi hayo huku akitangaza hatua kadhaa kufuatia mashauriano na wadau wa sekta ya uchukuzi kutokana na mzozo unaoendelea wa mafuta.
Miongoni mwa hatua hizo, Rais alisema Wizara ya Uchukuzi itashirikiana na benki pamoja na taasisi za kifedha kutafuta njia za muda za kuwasaidia waendeshaji wa usafiri wanaokabiliwa na changamoto za ulipaji wa mikopo.
Pia, aliiagiza wizara hiyo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti Bima (IRA) kushughulikia migogoro inayohusiana na madai ya bima yanayoathiri waendeshaji wa magari ya umma.
Wakati huo huo, Rais aliamuru kufanyika kwa mapitio ya haraka ya Sheria ya Bima na Sheria ya Madalali wa Minada ndani ya miezi mitatu ijayo ili kuunda mfumo wa haki zaidi kwa wadau wa sekta ya uchukuzi.
Aidha, NTSA itaandaa mazungumzo na kampuni za usafiri wa kidijitali pamoja na madereva wao ili kuweka kanuni za kiwango cha chini cha nauli za teksi na kutatua migogoro ya muda mrefu katika sekta hiyo.
