Skip to content

Hatua za dharura zimeimarishwa kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini Kenya.

SSERIKALI ya Kenya imeimarisha hatua za dharura za kukabiliana na Ebola huku ikiweka timu za wataalamu wa afya katika hali ya tahadhari saa 24 kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.

Waziri wa Afya, Aden Duale, alisema serikali imeanzisha mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa dharura kupitia Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Umma, huku vituo vya operesheni za afya ya umma vikichukua tahadhari katika ngazi ya kitaifa na kaunti.

Alisema mfumo wa mtandaoni wa kufuatilia wasafiri unatekelezwa huku serikali ikiendelea kutambua mienendo ya watu katika maeneo yaliyo katika hatari kubwa mpakani.

Maabara maalum za kupima Ebola zimeandaliwa katika vituo vya KEMRI Kisumu, KEMRI Nairobi, Maabara ya Kitaifa ya Afya ya Umma.

Serikali pia imeimarisha ushirikiano na serikali za Uganda na DRC, Shirika la Afya Duniani (WHO), Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kituo cha Magonjwa Afrika (CDC Africa).

Turkana imeandaa Hospitali ya Kanam Kemer kushughulikia visa vinavyoshukiwa huku vituo vya kutenga wagonjwa vikianzishwa Lokiriama, Nadapal na Kalobeyei.

Kwa upande mwingine, Busia imeongeza ukaguzi katika mipaka ya Busia na Malaba, huku Homa Bay ikipeleka maafisa wa afya katika maeneo ya Sena na Mbita kandokando ya Ziwa Victoria.

Nakuru nayo imetajwa kuwa eneo la hatari kutokana na kuwa kitovu cha usafiri kinachohudumia zaidi ya kaunti sita jirani.

Hata hivyo, baadhi ya kaunti zimekiri kuwa miundombinu iliyotumika wakati wa janga la corona imevunjwa au kubadilishwa matumizi, hali inayotatiza maandalizi ya sasa.

Mlipuko huo unahusisha aina ya Bundibugyo, mojawapo ya aina hatari zaidi za Ebola ambayo haina chanjo wala tiba iliyoidhinishwa.

Dalili za awali ni homa, maumivu makali ya kichwa, uchovu kupita kiasi na macho kuwa mekundu.

Kadri ugonjwa unavyoendelea kusambaa, mgonjwa anaweza kupata maumivu makali ya koo, kifua na tumbo pamoja na kutapika na kuharisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *