Taifa la Somalia linatarajiwa kushuhudia ukuaji hafifu wa uchumi kwa mwaka wa tatu mfululizo huku kupanda kwa bei za mafuta duniani kukiongeza shinikizo kwa uchumi wa nchi hiyo ambao tayari uko katika hali ngumu.
Ripoti ya hivi karibuni ya Benki ya Dunia kuhusu uchumi wa Somalia inaonyesha kuwa uchumi wa nchi hiyo utakua kwa asilimia 2.8 mwaka huu, ukishuka kutoka asilimia 3 iliyorekodiwa mwaka jana.
Huu utakuwa mwaka wa tatu mfululizo kwa Somalia kushuhudia ukuaji mdogo wa uchumi baada ya kurekodi asilimia 4 ya pato la taifa (GDP) mwaka 2023 na 2024.
Kulingana na Benki ya Dunia, ukuaji hafifu wa mwaka huu utachangiwa na kupunguzwa kwa misaada, mabadiliko ya tabianchi, mishtuko ya bei za bidhaa duniani pamoja na uwezo mdogo wa uzalishaji.
Benki hiyo, imesema kupunguzwa kwa misaada kwa taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kumesababisha athari kubwa za kijamii, huku ukosefu wa chakula ukiongezeka na juhudi za kupunguza umaskini kusimama.
Benki hiyo pia imeeleza kuwa matarajio ya uchumi wa muda mfupi na wa kati yamedhoofika zaidi kutokana na ongezeko la hivi karibuni la bei za mafuta duniani ambalo limeongeza changamoto nyingine kwa uchumi wa Somalia.
Kutokana na mabadiliko ya bei za bidhaa duniani, taifa la Somalia ambalo hutegemea sana uagizaji wa chakula na mafuta kutoka nje, pamoja na changamoto za usambazaji wa ndani zinazohusishwa na hali ya hewa na usalama, kiwango cha mfumuko wa bei kinatarajiwa kupanda hadi asilimia 6 mwaka huu kutoka asilimia 3.7 mwaka jana.
Hata hivyo, pato la taifa la Somalia linatarajiwa kuongezeka hadi asilimia 3.1 mwaka ujao kutokana na kuimarika kwa uwekezaji, ongezeko la fedha zinazotumwa kutoka nje pamoja na upanuzi wa miji.
