Takriban familia 1,000 zilizoathiriwa na mafuriko ya hivi karibuni katika kaunti ya Garissa zimepokea msaada wa bidhaa zisizo za chakula kutoka Shirika la Kenya Red Cross.
Msaada huo unalenga kupunguza mateso ya waathirika waliopo katika kambi za wakimbizi wa ndani huku wakisubiri maji kupungua ili waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida.
Waathirika hao wanatoka maeneo ya Bulla Punda, Bulla Kamor, Bulla Sheikh, Bakuyu na Ziwani na kwa sasa wamehifadhiwa katika kambi za Farmer Training Centre (FTC), Hyuga na Police Training Centre.
Akizungumza wakati wa ugawaji wa misaada katika kituo cha Farmer Training Centre Garissa, Mratibu wa Kenya Red Cross katika kaunti ya Garissa Ahmed Daud aliwataka wakazi hao kudumisha usafi wa mazingira na kutumia vyandarua vyenye dawa ili kuzuia mlipuko wa magonjwa kambini.
Wakati huo huo, Daud aliwataka wadau wengine kujitokeza kutoa msaada zaidi kwa familia ambazo bado hazijafikiwa, akisema bado kuna idadi kubwa ya watu wanaohitaji msaada wa dharura.
Mmoja wa walionufaika, Abubakar Hamisi, alisema misaada hiyo imefika kwa wakati mwafaka hasa vyandarua na blanketi kwani wengi wamekuwa wakikumbwa na baridi usiku pamoja na mbu ambao wanaweza kusababisha magonjwa.
Mafuriko katika kaunti za Garissa na Tana River, hasa maeneo ya kandokando ya Mto Tana, yalianza kufuatia mvua za msimu wa Machi hadi Mei ambazo ziliongeza kiwango cha maji katika mabwawa ya juu na kusababisha kuachiliwa kwa maji kwa njia ya kudhibitiwa
