Seneti imeibua maswali kuhusu ushahidi wa matibabu uliowasilishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika kesi ya kuondolewa kwake mamlakani.
Kupitia kwa Karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye, Seneti pamoja na Spika Amason Kingi wamehoji uhalali wa stakabadhi za hospitali zilizowasilishwa na daktari wa moyo Daniel Gikonyo.
Seneti inasema kuwa rekodi hizo zina utata na hazikuwahi kuwasilishwa mbele ya maseneta wakati wa kusikizwa kwa kesi ya kumbandua aliyekuwa naibu Rais Rigathi Gachagua mamlakani.
Daktari Gikonyo, aliambia mahakama kuwa Gachagua alilazwa hospitalini mwezi Oktoba 17 mwaka 2024 akiwa na maumivu makali ya kifua yaliyohitaji matibabu ya dharura.
Hata hivyo, Seneti sasa inadai kuwa ripoti hiyo inaonyesha Gachagua alikaa hospitalini kwa siku 31, jambo ambalo limezua maswali mapya kuhusu usahihi wa ushahidi huo.
Aidha, Seneti imehoji sababu iliyowafanya mawakili wa Gachagua kutowasilisha stakabadhi hizo wakati wa kusikizwa kwa kesi hiyo licha ya kuahidi kufanya hivyo.
