Skip to content

TAHADHARI MPYA YA MAFURIKO TANA RIVER

Gavan wa Tana River Dhadho Godhana pamoja na kamishna wa kaunti hiyo,Joseph Mwangi wametoa tahadhari kali kwa wakazi wanaoishi maeneo ya mabondeni na karibu na Mto Tana kuhama mara moja kuelekea maeneo ya juu kutokana na hatari ya mafuriko makubwa yanayotabiriwa katika siku na wiki zijazo.

Onyo hilo linajiri huku kina cha maji ya mto huo kikizidi kuongezeka kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo ya juu ya mlima Kenya na sehemu nyingine za vyanzo vya mto.

Serikali ya kaunti imesema tayari imeandaa maeneo salama ya muda na kambi za dharura kwa ajili ya familia zitakazoathirika.

Gavana Godhana amesema kuna uwezekano mkubwa wa KenGen kuanza kuachilia maji ya ziada kutoka mabwawa yake wakati wowote ili kudhibiti viwango vya maji, hatua ambayo inaweza kuongeza kasi ya mafuriko katika maeneo ya chini ya mto.

Serikali imeahidi kuwapatia wahanga chakula, blanketi, matandiko, huduma za afya pamoja na msaada mwingine wa dharura huku mipango ya kuwahamishia katika vijiji salama ikiendelea.

Aidha, serikali ya kaunti imetangaza kuwa mwezi huu utaanza ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa jamii ambazo huathiriwa mara kwa mara na mafuriko.

Kwa upande wake, Kamishna Mwangi amewataka wakazi kutii maagizo ya kuhama bila kusubiri hali kuwa mbaya zaidi.

Amesema machifu na wasaidizi wao wamepewa jukumu la kuhakikisha familia zilizo hatarini zinaondolewa mapema. Pia amewataka wafugaji kuhamisha mifugo yao kutoka maeneo ya kingo za mto.

Wakati huo huo, shirika la Kenya Red Cross limeendelea na shughuli za uokoaji katika maeneo yaliyozingirwa na maji, hasa eneo la Galedertu ambapo familia zaidi ya 81 zimeripotiwa kuathirika. Shirika hilo limesema kuwa mahitaji ya dharura ni pamoja na chakula, huduma za matibabu, vyandarua na maji safi kutokana na kuongezeka kwa hatari ya magonjwa ya mlipuko.

Tahadhari hiyo pia, imepanuliwa kwa wakazi wa kaunti za Garissa na Tana River kufuatia ongezeko la kina cha maji ya mito.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *