Wizara ya Afya imetoa wito wa kuoanisha mitaala katika taasisi za mafunzo ya afya nchini huku ikisisitiza umuhimu wa kuimarisha uwekezaji wa pamoja ili kukabiliana na upungufu wa wahudumu wa afya unaochangiwa na wimbi la wataalamu kuhamia mataifa ya nje kutafuta ajira.
Akizungumza siku ya Jumatano katika mazungumzo ya ngazi ya juu na Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Ulaya, Dr. Ouma Oluga alisema kuna haja ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kuhusu wafanyakazi wa afya, mikakati ya kuwabakiza kazini pamoja na mifumo ya uhamaji wa kitaaluma inayozingatia maadili kati ya Afrika na Ulaya.
Dr. Oluga alieleza kuwa masuala makuu yaliyojadiliwa ni pamoja na ajira za kimataifa zinazofuata maadili, changamoto katika utekelezaji wa makubaliano ya ajira kati ya nchi mbalimbali pamoja na ongezeko la wataalamu wa afya wanaohama kwenda nje ya nchi.
Mazungumzo hayo yalilenga kuendeleza mfumo wa ushirikiano wa wafanyakazi wa afya unaolenga kukabili upungufu wa wataalamu wa afya duniani, kuboresha mazingira ya kazi, kukuza ujumuishaji wa kijamii pamoja na kuimarisha ulinzi dhidi ya unyanyasaji na uchovu kazini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Ulaya Dr. Hans Kluge alieleza kuwa bara la Ulaya linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa umri wa wafanyakazi wa afya, visa vya ukatili dhidi ya wahudumu wa afya pamoja na matatizo ya afya ya akili na uchovu wa kazi.
Aidha, viongozi hao walijadili mpango wa kuanzishwa kwa Kituo cha Afrika cha Masuala ya Wafanyakazi wa Afya kitakacholenga kuimarisha mifumo ya afya kupitia mageuzi ya sera, mafunzo maalum, usimamizi wa uhamaji wa wataalamu pamoja na ustawi wa wafanyakazi wa afya.
Mazungumzo hayo yameonyesha umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya Afrika na Ulaya katika kujenga mfumo imara wa afya wenye wafanyakazi walio salama, wenye motisha na uwezo wa kukabiliana na changamoto za afya duniani siku zijazo.
