Chama cha Orange Democratic Movement, ODM, kimeanza mikakati ya ndani ya kujitathmini kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 huku kukionekana wasiwasi kuhusu hatima ya chama hicho bila Raila Odinga kuwania urais.
Kupitia tangazo rasmi, ODM imewaalika wanachama wanaotaka kuwania nyadhifa mbalimbali kupitia tiketi ya chama hicho kuwasilisha maombi yao kabla ya mwezi Juni tarehe 30.
Hatua hiyo inalenga kupima ushawishi wa chama hicho katika maeneo mbalimbali nchini huku viongozi wake wakitaka kurejesha imani ya wanachama katika mchakato wa kura za mchujo.
Kwa mara nyingine, ODM imekabiliwa na mgawanyiko wa ndani kuhusu iwapo imuunge mkono Rais William Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2027.
Viongozi wa chama wanaamini kuwa mafanikio ya ODM yatategemea uwezo wake wa kuhakikisha kura za mchujo zinafanyika kwa haki, uwazi na bila malalamiko ya udanganyifu.
