Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka,nchini IEBC, imeonya kuwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027 huenda yakatatizika kutokana na uhaba mkubwa wa fedha.
Naibu Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Obadiah Keittany, amesema kuwa IEBC inahitaji jumla ya shilingi bilioni 74 nukta 8 kuendesha uchaguzi huo, lakini hadi sasa imetengewa shilingi bilioni 41 nukta 3 pekee, hali iliyozua pengo la zaidi ya shilingi bilioni 33.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Sheria, Keittany alisema ongezeko la bajeti limetokana na matarajio ya kuongezeka kwa idadi ya wapigakura kutoka milioni 22 mwaka 2022 hadi zaidi ya milioni 28 mwaka 2027.
Aidha, vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kuongezeka kutoka elfu 46 hadi elfu 55 kote nchini.
Kamishna wa IEBC Profesa Francis Aduol amesema kuwa tume hiyo inalazimika kubadilisha vifaa vyote vya KIEMS vilivyotumika katika uchaguzi uliopita kwa kuwa vimepitwa na wakati.
